Uongozi wa Simba SC umeendelea kupewa ushauri na kukosolewa kwa baadhi ya mambo ambayo yanadaiwa kuwa chachu ya kushindwa kufikia malengo wanayojiwekea kila msimu katika Michuano ya ndani na ile ya Kimataifa.

Simba SC kwa misimu miwili mfululizo imeshindwa kurejesha ubingwa wa Tanzania Bara uliopotelea mikononi mwa watani zao wa jadi Young Africans, huku ikishindwa kuvuka hatua ya Robo Fainali katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa msimu mitano.

Mchambuzi Mkongwe wa Soka nchini Tanzania Edo Kumwembe, ni sehemu ya wadau waliotoa ushauri na kukosoa taratibu zinazotumiwa na Uongozi wa Simba SC, katika kufikia mipango na mikakati yao kwa kila msimu.

Edo amesema kwa muda mrefu Uongozi wa Klabu hiyo ya Msimbazi, umeshindwa kutambua tatizo linalowakabili na kujikuta ukirudia kosa lile lile, hivyo anaamini ni wakati mzuri kwao kujitafakari.

Hata hivyo Ushauri wa Mchambuzi huyo, umetumia mifano mingi kwa kuitaja Young Africans ambayo imekuwa na muendelezo mzuri wa kwenye michuano ya ndani na ile ya Kimataifa, ambapo msimu uliopita ilicheza Fainali Kombe la Shirikisho huku msimu huu ikikaribia kucheza Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

“Na sasa ni muda wa Simba kujitafakari. Wanatoka wapi na wanakwenda wapi? Young Africans aliingia fainali za Shirikisho msimu uliopita na msimu huu ilibakia kidogo waende Nusu Fainali za Ligi ya mabingwa. Wana timu bora ambayo ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya ndani msimu huu na ina viongozi vijana ambao wanakwenda kasi”

“Simba waige hili. Kutolewa pamoja na Young Africans kusiwe faraja kwa Simba, bali waangalie mfumo wao wa kuingiza wachezaji klabuni. Simba inapaswa kurudi kule kwenye njia yake ambayo waliitumia hadi wakaweza kuongoza kundi lililokuwa na timu kali za kina Al Ahly na AS Vita. Kwa sasa unaona wazi kwamba makali yale hayapo na bahati mbaya kuna viongozi ndani ya Simba wanaona kama vile Young Africans wanabahatisha”

“Fitina za mpira katika Afrika zipo lakini unahitaji kuwa na timu bora. Ubora haujifichi uwanjani. Young Africans walikuwa na kina David Molinga wakaishia kulalamika kwamba TFF walikuwa wanaibeba Simba. Sasa hivi wamekuwa na timu bora wamekaa kimya wakati uongozi wa TFF umeendelea kuwa ule ule tu”

“Tusubiri kuona nini kitaendelea kuanzia sasa mpaka mwisho wa msimu na kisha katika dirisha la usajili. Kuna kitu lazima kibadilike kabla lawama hazijaanza kumshukia kocha Abdelhak Benchikha. Anaonekana kuwa na rekodi nzuri katika timu alizotoka lakini ni wazi kwamba alikuwa anasaidiwa pia na ubora wa wachezaji.”

Ufanisi: Tatueni changamoto za Wafanyakazi - Dkt. Kiruswa
Saba wafariki kwa ajali ya Daladala, mmoja mahututi