Bondia wa kimataifa wa Tanzania, Yusuf Changalawe ameahidi kupambana hadi kufuzu Michezo ya 33 ya Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa mwaka huu.
Changalawe ameyasema hayo wakati akirejesha bendera ya taifa kwa Kamati ya Olimpiki ya Taifa (TOC) baada ya kushiriki mashindano ya kwanza ya dunia ya kufuzu Olimpiki yaliyofanyika Milan, Italia.
Amesema kuwa anaishukuru sana TOC kwa kufanikisha kushiriki mashindano hayo ya Italia, licha ya kushindwa kufuzu baada ya kutolewa katika hatua za awali.
Bondia huyo wa Light heavy ameiomba TOC kuendelea kuwa na imani naye na kumuunga mkono katika jaribio jingine la kufuzu kwa olimpiki litakalofanyika Bangkok, Thailand kuanzia Mei 23 hadi Juni 3, 2024.
Changalawe kabla ya kushiriki jaribio la kwanza la dunia Milan, Italia, alishiriki lile la Afrika lililofanyika Dakar, Senegal kuanzia Septemba 9 hadi 15, 2023.
Akizungumzia mashindano ya Italia, Changalawe amesema kuwa pamoja na kushindwa, alifanya vizuri lakini waamuzi walimuangusha.
Ameliomba Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) kujitahidi kupeleka waamuzi na majaji katika mashindano mbalimbali ya kimataifa kama zinavyofanya nchi nyingine, kwani inaweza kusaidia mabondia wa Tanzania pia kupata haki.