Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi, amesema watakuwa makini katika mchezo wao wa hatua ya 16-bora wa Kombe la CRBD Bank dhidi ya Dodoma Jiji FC, kwani ni timu iliyowasumbua kwenye mechi ya Ligi Kuu, huku akihofia wachezaji wake kubweteka baada ya kutoka kucheza michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kikosi cha Young Africans kiliwasili jana jioni jijini Dodoma kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kesho Jumatano (Aprili 10) kwenye dimba la Jamhuri, jijini humo.

Akizungumza jijini Dodoma, Gamondi amesema wamejipanga Vizuri kulingana na mchezo huo kuwa mgumu kwani mashindano hayo ni mtoano na anayefungwa anatoka.

Amesema walipata muda mfupi wa kufanya mazoezi kwa sababu ya kutoka katika mashindano makubwa na anatambua Dodoma Jiji FC mara ya mwisho iliwasumbua.

“Haitakuwa mechi rahisi kwa sababu Dodoma Jiji FC ni wazuri na tuliwahi kucheza nao nyumbani na walitusumbua, mchezo huu tunatakiwa kuwa makini na kucheza kwa tahadhari kubwa ili kufuzu kucheza Robo Fainali,” amesema Gamondi.

Ameongeza kuwa wanahitaji kutetea mataji yao yote msimu huu na ili kufanikisha malengo yao ni kushinda mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji FC na kwenda kucheza Robo Fainali na baadae nusu na kisha fainali.

Gamondi amesema licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali, lakini anaimani na wachezaji waliopo fiti kwa mchezo huo kwenda kupambana na kupata matokeo mazuri mbele ya wapinzani wao hao.

Young Africans itashuka dimbani kesho Jumatano (April 10) ikitoka kupoteza kwa mikwaju ya Penati 3-2 dhidi ya Mamelodi Sundowns kwenye mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa nchi Afrika Kusini ljumaa iliyopita (Aprili 05).

Mechi hiyo ilifikia changamoto ya mikwaju ya Penati baada ya matokeo ya suluhu kwa dakika zote 90 za nyumbani na Ugenini.

Changalawe aahidi kufuzu olimpiki 2024
Serikali kutoa taarifa tathmini ya Mazingira