Boniface Gideon – Tanga.
Wimbi kubwa la watoto wa mtaani na yatima limekuwa likiongezeka likidaiwa kusababishwa na Jamii kushindwa kutekeleza wajibu wao na uwepo baadhi ya Mila na Desturi zinazopelekea Watoto kushindwa kupata haki za msingi.
Akizungumza na wadau mbalimbali wakati wa hafla yakula chakula na Watoto Yatima, Mkurugenzi wa kituo cha kulea watoto wa Yatima cha Goodwill Children’s home Seyyed Idarus, alisema pia wazazi kushindwa kuvumiliana pamoja na ndugu kuwatelekeza watoto pale wanafamilia wanapofariki kumesababisha ongezeko hilo.
Amesema, “ndugu zangu mliopo hapa na wale mliopo majumbani, niwaambie tu kuwa chanzo kikubwa cha watoto wa mtaani pamoja na yatima inatokana na mifarakano ya wazazi ni chanzo kikubwa cha watoto wa mtaani, lakini pia ndugu na jamaa kushindwa kutimiza wajibu wao pale wazazi au Walezi anapofariki, hali sio nzuri kabisa.”
Kwa upande wake mlezi kutoka kituo cha Watoto Yatima Casade la Joiya kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki, Caroline Bundi alisema kazi ya kulea Watoto ni nzito hivyo Jamii inahitaji kushikamana.
“Chukulia Watoto wachache unaowalea hapo nyumbani unavyohangaika nao, sasa sisi wenzenu tunawalea watoto wengi zaidi, ambao hatujui Mila na Desturi zao, ni kazi inayohitaji moyo, tunaomba tusaidiane katika malezi ili Watoto hawa wapate haki zao za msingi na baadaye waje waisaidie Jamii,” alisema Caroline.