Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa ameitaka Idara ya Afya ya Ofisi hiyo kufika kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kufanya tathmini ya mahitaji ya maboresho ya miundombinu ya afya ili wananchi wapate huduma za afya.
Mchengerwa ametoa kauli hiyo katika Kijiji cha mloka Kata ya Mwaseni kwenye ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo kutoa pole kwa wananchi walioathiriwa na mafuriko katika kata 12 za Wilaya hiyo.
Kauli hiyo ya Mchengerwa imetokana na ombi la Diwani wa kata hiyo Mhe. Saadina Malenda ambaye ameomba upatikanaji wa Mtaalamu wa Kutoa Dawa ya Usingizi katika kituo cha Afya Mloka ili kituo hicho kitoe huduma upasuaji wa dharura kwa wananchi wa eneo hilo na ameaagiza Idara hiyo kufika mapema wiki ijayo na kufanya tathmini hiyo na kumshauri ili fedha zipelekwe kulingana na mahitaji.
Amesema, “nataka kuona kituo hiki kinatoa huduma zote muhimu za afya, wananchi wa Kata ya Mwaseni waweze kunufaika na huduma bora za Afya, hapa kilipo katika kijiji cha Mloka ni eneo muhimu kwa sababu kinakutabisha watu wengi kutoka maeneo mbalimbali hivyo na huduma za Afya lazima ziwe za viwango, pia fikeni kata ya Kipugila, Ngorongo na pamoja na Mkongo.”
Wakati huo huo, Mchengerwa amekabidhi gari ya kubebea wagonjwa (Ambulace) katika Kata ya Mwaseni ambayo itakua ikiwezesha kubeba wagonjwa kutoka kata hiyo na kuwapeleka kwenye Hospitali ya Wilaya kutokana na Halmashauri hiyo kukumbwa mafuriko na Kata 12 kati ya 13 ziliathiriwa na kusababisha adha kubwa kwa wananchi zaidi ya 89,000.