Mshambuliaji Darwin Nunez amechochea moto uvumi wa yeye kuondoka Liverpool majira ya joto baada ya kufuta picha zote za akiwa na klabu hiyo kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram.
Ripoti kutoka nchini England zinasema kuwa Nunez, ambaye inasemekana anaweza kuuzwa msimu huu wa majira ya joto huku Barcelona ikiwa na nia ya kumsajili, kwani inatafuta mbadala wa muda mrefu wa Robert Lewandowski.
Baada ya tetesi hizo kuanza kuibuka, Nunez aliachwa nje ya kikosi cha kwanza Liverpool kilichoshinda mabao 4-2 dhidi ya Tottenham Hotspur mwishoni mwa juma lililopita, akitokea benchi kwa dakika 15 za mwisho.
Uvumi huo uliongezeka baada ya filimbi ya mwisho wakati Nunez alipoondoa kila picha inayohusiana na Liverpool kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram.
Ukurasa wa Nunez bado unajumuisha picha za wakati akiwa Benfica, lakini kinachofuata ni machapisho kuhusu familia yake au Timu ya Taifa ya Uruguay.
Liverpool walilipa Pauni Milioni 85 kumnunua Nunez kutoka Benfica mwaka 2022 na ripoti zinaonesha tayari wamelipa jumla ya Pauni Milioni 76.5, huku Pauni Milioni 8.5 zilizosalia zikihusishwa na vipengele ambavyo havijabainishwa kuhusiana na uchezaji wa timu na mtu binafsi.
Kutokana na hali hiyo, Nunez ndiye mchezaji aliyeweka rekodi ya kusajiliwa na Liverpool, akipita Pauni Milioni 75 zilizolipwa kumsajili beki wa kati Virgil van Diik, lakini Mashabiki wengi wa wekundu hao wanaona hawajaona thamani ya gharama yao kubwa.