Licha ya timu yake kuburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amesema wataendelea kupambana hadi mechi yao ya kufunga pazia ya msimu na wanaamini huenda mambo yakabadilika.
Mtibwa Sugar sasa inajiandaa kuikaribisha Tabora United, mechi itakayochezwa kesho Alhamis (Mei 09) kwenye Uwanja wa Manungu Complex ulioko Turiani, Morogoro.
Katwila amesema licha ya kupoteza mechi, wachezaji wake wanajitahidi kupunguza makosa jambo ambalo anaamini wanaweza kujinasua katika janga la kushuka daraja.
“Ni kweli unapopoteza mechi hali inakuwa ngumu, lakini hayo ndio matokeo ya mpira, hatua ambayo tupo hakuna mechi inayotabirika, kila timu inapambana kusaka matokeo mazuri, sisi pia hatujakata tamaa, ni upepo tu bado hauko vizuri upande wetu,'” amesema Katwila
“Hatutawadharau Tabora United, kila timu iko katika hali mbaya, tutaingia uwanjani kwa tahadhari, kwa sasa hakuna kusema unacheza nyumbani au ugenini, tuko vitani,” ameongeza kocha huyo.
Mendy kulamba dili jipya Real Madrid
Baada ya juzi Jumatatu (Mei 06) kuchapwa mabao 2-0 wakiwa nyumbani, Mtibwa Sugar imeendelea kuburuza mkia ikiwa na alama 17 wakati mabingwa watetezi Young Africans wakiendelea kujiimarisha kileleni.