Katika jiji la Cluj-Napoca Nchini Romania, raia wanaweza kupata bure tiketi ya basi ikiwa watafanya zoezi la kuruka kichurachura mara 20 mbele ya kibanda maalum, wakilenga kupunguza matumizi ya magari binafsi, kuhimiza raia kutumia usafiri wa umma na kukuza utamaduni wa kufanya mazoezi, ili raia wawe na afya bora.
Zoezi hilo lilianza mwishoni mwa Desemba 2023, na wahusika hupatiwa zawadi ya Tiketi ya Afya bure ikifahamika kwa jina la (Biletul de Sănătate) ikiwa ni uzinduzi wa kampeni yaTamasha la Michezo lililoendeshwa ambapo watu wa Cluj Napoka walifanya zaidi ya miruko ya kichurachura milioni 1 katika siku 99.
Hata hivyo, inaarifiwa kuwa lengo la kufanya hivyo, si tu kuwafanya watu wafurahie tiketi ya bure ya basi, lakini pia kuwatia moyo ili wafuate mtindo bora wa maisha wa kujishughulisha zaidi hata kuamua kufanya mazoezi ya viungo kuwa ni sehemu ya utaratibu wao wa kila siku.
Hii si mara ya kwanza kwa watu kuweza kushiriki mazoezi ya viungo kwa ajili ya safari za bila malipo, kwani katika Michezo ya Olimpiki wakati wa majira ya baridi huko Sochi mwaka wa 2014, watu walitakiwa kuchuchumaa ili kupata tiketi za treni bila malipo katika kituo cha magharibi mwa Moscow.
Aidha, mnamo Februari 2020 pia Shirika la Indian Railways liliweka kibanda cha kuchuchumaa kama sehemu ya mpango wa nchi hiyo kuwafanyisha watu mazoezi kupitia kampeni waliyoiita ‘Fit India’ wakilenga kukuza mazoezi ya mwili na kutumia usafiri wa umma kama ushindi maradufu kwa afya ya jamii.