Aliyewahi kuwa mtathmini wa video na viwango wa Klabu ay Al Nassr ya Saudi Arabia ambayo kwa sasa anachezea Cristiano Ronaldo, Alexandre Kerveillant amewasilisha maombi mezani kwa Simba SC akitamani kupewa kazi hiyo ambayo kwa sasa inafanywa na Mzimbabwe, Culvin Mavunga.
Baada ya kupata fununu kuwa Simba SC kwa sasa inafanya tathmini ya utendaji kazi wa Mavunga kuona kama imfungulie milango au ibaki naye,
Kerveillant amewasha kompyuta yake mpakato ‘Laptop’ fasta kisha akatupa barua pepe kwa uongozi wa Simba SC akiwapa wasifu wake mrefu unaoonyesha uzoefu wa kutosha alionao wa kazi hiyo.
Kerveillant ambaye pia ni kocha mwenye leseni ya juu umoja wa vyama vya mpira wa miguu Ulaya ‘UEFA’, miezi miwili iliyopita aliachana na Nantes inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa ambayo alikuwa akiitumikia katika majukumu hayo akimsaidia Antoine Kombouare.
Mfaransa huyo ana wasifu ulioshiba wa kazi ya kutathmini viwango na video kwenye timu na ushuhuda wa hilo ni timu ambazo amewahi kuzifanyia kazi kwa nyakati tofauti.
Kabla ya kujiunga na Nantes, Kerveillant aliitumikia Al Nassri inayoshiriki Ligi ya Saudi Arabia katika msimu wa 2022/2023 akimsaidia Rudi Garcia kabla ya kuachana nayo Aprili 13, 2023.
Ukiondoa Al NasSr, Kerveillant katika msimu wa 2021/2022 aliitumikia FC Sion ya Switzerland chini ya makocha wawili tofauti ambao ni Paolo Tramezzani na Marco Walker na timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.
Ikumbukwe kabla ya hapo mtathmini huyo wa viwango alidumu kwa misimu miwili katika timu ya Beijing Guoan inayoshiriki Ligi Kuu ya China akiwa anamsaidia kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Croatia, Slaven Bilic.
Mbali na Slaven Bilic na Rudi Garcia, makocha wengine wakubwa waliowahi kufanya kazi na Keirvellant ni Leonardo Jardim na Thierry Henry ambao aliwasaidia katika klabu ya AS Monaco.