Kujiuzuru kwa Zitto Kabwe ndani ya Chama cha ACT-Wazalendo ni alama ya kuonesha ukomavu wa kisiasa na kuheshimu utaratibu uliowekwa, hatua ambayo inatoa mwanya wa Viongozi kupokezana madaraka kwa minajili ya kujenga chama, bila kuwa na nia ya kumfukuza yeye au yeyote, kwani siyo ndoto zao.
Hayo yamebainishwa na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Dorothy Semu wakati akifanya mahojiano maalum katika Studio za Dar24 Media zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam na kudai kuwa utaratibu huo pia unajenga taasisi inayoamini kwenye ukomavu wa uongozi na imani kwa kila mwenye sifa ya kuongoza.
Amesema, “ni alama kwake, ni alama kwa taasisi katika mafanikio ya uongozi bila kujali aliyepo sasa ni bora sana na wengine hawataweza, tunaamini kwamba tunajenga taasisi ambayo wakati wowote Viongozi watakuwa tayari kupokezana uongozi na kuendeleza ujenzi wa taasisi inayoamini katika kupokezana uongozi na kuendeleza malengo yetu ya kitaasisi.”
Akijibu swali la Mwandishi Stanslaus Lambat, iwapo wana uwezo wa kumfukuza uanachama Zitto Kabwe endapo ataenda nje ya matakwa ya ACT Wazalendo, Doroth amesema adhabu ya kumfukuza mtu uanachama ni ya mwisho na haitekelezwi kwa urahisi kutokana na historia ya chama hicho.
“Tunaamini sisi ni Viongozi na kazi yetu ni kulea, kazi yetu ni kuboresha mwanachama au kiongozi yoyote ndani ya chama na kumfukuza mtu kwenye chama iwe ni kitu cha mwisho kabisa baada ya kushindikana kwa hatua nyingine zote kwahiyo sisi kama viongozi siyo ndoto yetu kumfukuza mtu yeyote uanachama,” amesema Dorothy.
Kuhusu mtafaruku ambao ulijitokeza na kupelekea baadhi ya Viongozi kuondoka kwenye chama akiwemo Hamad Masoud, Kiongozi huyo wa ACT alikiri kutokea tofauti hiyo na kusema ilikuwa ni baada ya uchaguzi ambapo watu hao walisema hawakutendewa haki, lakini chama hakikumfukuza yeyote.
“Na baadhi ya wanachama ambao waliondoka na yule ambaye alilalamikia kutotendewa haki wengi wamerudi ndani ya chama, wamejua ilikuwa ni mpito ni joto la uchaguzi na hii imekuwa kawaida kwenye vyama vya siasa pale watu wanapohitilafiana wengine huhisi muafaka ni kutoka na sisi tunaheshimu pale mtu anapoona atoke tukiwa na uelewa kwamba joto la uchaguzi huja na mambo mengi,” alisema Dorothy.