Johansen Buberwa – Kagera.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya Missenyi Mkoani Kagera, wameiomba Kamati ya usalama kuingilia kati wizi wa Kahawa pamoja uuzwaji wa Kahawa Mbichi za Butura kimagendo, ili kusaidia kukuza uchumi wa Wakulima na Wilaya hiyo.
Wakizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa za Kata 20 za Wilaya hiyo kwenye robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/2024, Diwani wa Kata ya Ishozi, Robert Karwa na Rafiu Abeid wa Kata ya Ruzinga wamesema baadhi ya Wakulima wa zao hilo na wanunuzi huumia njia zisizo rasmi kibiashara.
Aidha, wamemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwahimiza watendaji wa Vijiji na Wenyeviti kushughulikia suala hilo bila kuwaogopa Viongozi watakaobainika kuhusika ili Wakulima wasiendelee kuibiwa.
Kufuatia hali hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Missenyi Wille, Mutayoba ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuingilia kati ili kuwanusuru Wakulima kwa kukamata wezi watakao husika na wizi wa Kahawa na wauzaji wa Butura.