Kiwango cha Wachezaji Chipukizi Ladack Juma Chasambi na Edwin Balua kimemkuna Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda na kujikuta akifichua jambo kwa wawili hao.
Chasambi na Balua wamekuwa wakipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Simba SC tangu Mgunda alipotangazwa kukaimu nafasi ya Kocha Mkuu, kufuatia kuondoka kwa Abdelham Benchikha ambaye alikuwa hawapi nafasi wachezaji hao wazawa.
Akizungumza jijini Dar es salaam Mgunda ambaye amekuwa na matokeo mazuri tangu aliporejea kwenye Benchi la Ufundi la Simba SC amesema, Wajibu na Kujituma ndio siri kubwa ya kuwaamini wachezaji hao waliosajiliwa klabuni hapo wakati wa Dirisha Dogo.
“Wale Wachezaji Vijana ni Wachezaji wa Simba SC, wamesajiliwa na Simba SC na katika kusajiliwa kuna mambo mawili, Haki na Wajibu, mimi ninawapa nafasi ili watimize Wajibu wao, ninachoshukuru ni kwamba wanatimiza wajibu wao vizuri na Mungu awabariki na ninaamini kabisa huko tuendako watazidi kutimiza wajibu wao vizuri zaidi.”
“Huwezi kuamini tuna majeruhi karibu sita ambao wote wanacheza katika kikosi cha kwanza, tuna Kibu, Saido, Chama, Babakar Sar na wengine, kwa hiyo utaona kwamba ni jinsi gani gepu lilivyokuwa kubwa, lakini ninachoshukuru ni kwamba hawa vijana tuliowapa nafasi wamethibitisha kwamba kwa nini walisajiliwa Simba SC, kwa hiyo ninawapongeza viongozi wangu kwa kuwasajili vijana hawa na hawakufanya makosa.” amesema
Mgunda pia akafafanua kwa nini amekuwa na mafanikio katika kipindi kifupi tena kwa kuwatumia wachezaji wale wale ambao walionekana kuwa katika kiwango cha kawaida wakati wa utawala wa Kocha Benchikha aliyeamua kuvunja mkataba wake klabuni hapo kwa shinikizo la matatizo ya kifamilia.
“Ninachofurahia wachezaji niliowakuta ambao wamesajiliwa na Simba SC ilikuwa ni muda tu ifike wakati kucheza, imefika wakati wangu nimewapa nafasi ya kucheza, lakini ni wachezaji wanaostahili kucheza, yote kwa yote ni wachezaji wa Simba SC na watakiwa kuitumikia Simba SC na niwajibu wao.” ameongeza Mgunda