Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameridhia ombi la Kanisa la Anglikana Tanzania la kutaka kuifanya Juni 6 ya kila mwaka kuwa siku maalum ya kumbukumbu kuondolewa biashara ya utumwa, huku akisamehe kodi ya makusanyo ya watalii eneo la kihistoria la Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati wa Ibada Kuu ya Upatanisho na Msamaha kutokana na madhila ya biashara ya utumwa iliyofanyika kwenye Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Zanzibar Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini, Mkoa wa Mjini Magharibi na kuongozwa na Askofu Mkuu wa Canterbury, Mhashamu Justin Welby hii leo Mei 12, 2024.
Amesema, pia Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi za Dini ili, ziweze kufanya shughuli zao kwa uhuru na kushirikiana kutoa huduma mbalimbali kwa jamii na kutatua changamoto zao.
Aidha, amewashukuru viongozi wa Madhehebu ya Dini kwa kuendelea kuhubiri amani, umoja na mshikamano na kuwahimiza waumini wote kudumisha tunu hizo muhimu kwa taifa letu.
Kufuatia Serikali kusamehe kodi ya makusanyo ya watalii eneo la kihistoria la Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini, Rais Dkt. Mwinyi ameiagiza Wizara ya fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya kushughulikia kwa utaratibu mzuri wa makusanyo katika eneo hilo.