Waganga wa tiba asili katika kaunti ya Kilifi Nchini Kenya, wameilaumu Serikali kwa kushindwa kuwatambua huku ikiwatenga katika juhudi za kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoikabili jamii.
Hayo yamebainishwa na Kiongozi Mwandamizi wa Wazee wa Kaya eneo la Pwani, Tsuma Nzai Kombe ambaye amesema wanaiomba Serikali kuwatambua na kuwashirikisha kikamilifu katika utafiti wa tiba mbalimbali za maradhi sugu, ikiwemo kifafa.
Amesema, “huduma za kiafya za kiasili hupatikana kwa kila jamii tangu enzi za mababu na zilisaidia kwa madhumuni ya kutambua, kukinga kutibu na kuboresha mwili kutokana na magonjwa pamoja na maradhi mbalimbali.”
Kombe ameongeza kuwa huduma hizo hutolewazo na watu wa aina mbalimbali kwa kutumia nyenzo, ujuzi na uzoefu wa kiasili, japo hutofautiana kijamii au kabila moja hadi jingine na hivyo kitendo cha Serikali kutowashirikisha ni kudharau nyenzo muhimu yenye msaada kwa jamii.