Kamanda wa kikosi cha Zima moto mkoa wa Pwani, Jenifa Shirima amekanusha dhana potofu ya baadhi ya watu katika jamii akisema hakuna gari la zimamoto linalofika kwenye tukio la kuzima moto bila kuwa na maji.
Shirima amekanusha madai hayo wakati akitoa mada kwenye hafla ya maadhimisho ya siku ya vyombo vya Habari duniani kimkoa, yaliyofanyika Wilayani Kibaha Mkoani Pwani ambapo wadau wa Habari walihudhuria na kutoa mada mbalimbali.
Amesema, “gari la zima moto hukaa kituoni likiwalimejaa maji kulingana na ujazo wa tanki tayari kwa safari ya kwenye tukio ambapo magari hayo ujazo wake huanzia lita 2000, 5000, 7000, 10,000, 15000 na kuendelea kulingana na ukubwa wa gari husika.”
“Kwa mfano gari letu la zima moto la wilayani Kibaha lina ujazo wa lita 7000 ambalo linaweza kumwaga maji hayo katika tukio la kuzima moto kwa muda wa chini ya dakika tano kwani kasi ya matumizi ya maji hutegemea ukubwa wa moto, aina ya moto na jinsi ambavyo yule anayeendesha mtambo,” aliongeza Shirima.