Hamida Kamchalla – Tanga.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Wanafunzi kati ya 600 hadi 700, ambao watafuzu vizuri masomo ya Sayansi na Hisabati na wenye nia ya kutaka kusoma Vyuo vya elimu ya juu vya ndani ya Nchi, watasomeshwa bure.

Prof. Mkenda ameyabainisha wakati akizindua maadhimisho ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyofanyika Kitaifa jijini Tanga na kudai kuwa Wanafunzi hao ni wale watakaosoma masomo ya Sayansi, Uhandisi, Tehama, Elimu tiba na Hisabati, ambao kwa asilimia 100 watalipiwa na Serikali.

Amesema, “siyo mikopo, Serikali itakulipia garama zote ikiwemo kujikimu, malazi na chakula mpaka umalize kusoma, ilimradi waendelee kufanya vizuri kwenye masomo yao kwenye vyuo wanavyosomea.”

Prof. Mkenda amebainisha kuwa, kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM, katika kuendeleza Sayansi na Teknolojia, Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan), aliagiza zitengwe fedha kwa ajili ya kuwasomesha vijana wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi.

Amesema, Serikali ipo katika mchakato wa kujenga shule 100 za mafunzo ya Amali katika nyanja ya ufundi nchi nzima, ili kuwawezesha vijana wa Kitanzania kuweza kujiajiri au kuajiriwa kupitia ujuzi watakaopata kupitia vyuo hivyo.

Prof. Mkenda pia amezindua rasmi mwongozo wa Samia Scholarship kwenda kusomea elimu ya juu ya nyuklia nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuongeza madirisha ya wahitaji  na kusema maonesho hayo ni chachu ya maendeleo kwa sekta ya elimu katika ubunifu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Elimu, Michezo na Utamafuni, Husna Sekiboko akiongea na Wananchi kwenye maadhimisho hayo.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema ili kuendana na kasi ya maendeleo Duniani inapasa kufanya mabadiliko makubwa ya sayansi na tekinolojia

Amesema, “Dunia ya sasa ina mabadiliko makubwa hasa kwenye masuala ya sayansi, tekinolojia, Ujuzi na Ubunifu, hivyo basi ni wakati wa vijana wa Kitanzania kwenda sambamba na mabadiliko hayo.”

Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Prof. Adolf Mkenda akielekeza jambo wakati akipita kwenye mabanda.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge – Elimu, Husna Sekiboko amesema Bunge linatamani kuona bunifu zinazoibuliwa zinaboreshwa Ili zilete tija na kutatua kero mbalimbali za kijamii.

“Maonesho haya yameibua fursa mbalimbali kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na wadau wa maendeleo ambayo wamejifunza tekinolojia mbalimbali za kisiasa katika kutekeleza majukumu yao” amesema Sekiboko.

OSHA watakiwa kuharakisha uchunguzi wa ajali Mtibwa Sukari
Ugomvi wa wanandugu wasababisha mauaji, wawili mbaroni