Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imekubali ombi la Mabalozi wa nchi mbalimbali walioomba kikao cha kujadili kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa lengo la kukwamua changamoto zinazowakabili wawekezaji kutoka nchi zao.
Mabalozi walioomba kikao na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na balozi wa Marekani, Uingereza, Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji, Canada, Korea, Sweden, na Ujerumani.
Akijibu ombi hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, alisema serikali ipo tayari kujadiliana na mabalozi hao kama walivyoomba, wakiamini kikao hicho kitakuwa na tija na kushughulikia changamoto zilizojitokeza.
“Nimekubali maombi yenu ya kikao kujadili changamoto mlizoziorodhesha na nitaandaa uwepo wa maafisa wa serikali kutoka taasisi husika kama mlivyoomba. Ili kikao kiwe na tija tunaomba wawekezaji mnaowazungumzia waje na vielelezo vya kina vya changamoto zinazowakabili,” alisema Waziri Makamba.
Aidha, Waziri Makamba amewahakikishia Mabalozi dhamira na nia dhabiti ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya kibiashara nchini, ili kuvutia uwekezaji kutoka nje (FDI) kama ambavyo imefanikiwa kufanya ndani ya muda mfupi kutoka uwekezaji wa Dola za Kimarekani Bilioni 3 mwaka 2022 mpaka Bilioni 5.5 mwaka 2023.