Penina Malundo
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jaffo amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji nchini ili kuweza kupata fursa ya kuwekeza vizuri na kufanya biashara zao.
Amesema ushirikiano kati ya nchi ya Tanzania na China, umeweza kusaidia kuwepo kwa faida nyingi ikiwemo mahusiano ya kiuchumi ambapo bidhaa zaidi ya dola za Kimarekani Bilioni 3.3 zinazosafirishwa kutoka Tanzania kwenda China na bidhaa zinazotoka China na kuja Tanzania zinafikia takribani dola za kimarekani Trilioni 3.5.
Akizungumza jana, wakati alipohudhuria Siku Maalum ya China ndani ya maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa “Sabasaba” yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere alisema ndani ya miaka 60 nchi ya Tanzania na China zimeweza kuwa na uhusiano pamoja na mashirikiano mazuri katika nyanja mbalimbali.
Alisema miongoni mwa uhusiano mwingine ulipo kati ya Tanzania na China ni pamoja na viwanda vya wachina ambavyo vimejengwa nchini na kutoa ajira kwa vijana wengi.
“Pia tunashuhudia kwenye upande wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali china kupitia wakandarasi wake wanaweza kufanya kazi kubwa sana za ukandarasi katika nchi yetu ,”alisema na kuongeza
“Katika maonesho haya ya Sabasaba makampuni zaidi ya 100 za China yameweza kushiriki katika maonesho haya na hii inamaana Tanzania inavutia uwekezaji wake ndani ya nchi yetu,”alisema.
Dk. Jaffo alihamasisha kuendelea kwa ushirikiano huo na kuwekeza ili kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa vijana kwani kila mwaka vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu na serikali haiwezi kuajiri vijana wote hivyo kuimarika kwa sekta binafsi itasaidia suala la ajira kwa vijana wa Kitanzania.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian alisema nchi ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika masuala ya biashara na uwekezaji ili kurahisisha ushirikiano kuzidi kuimarika.
“Tunaishuku Serikali ya Tanzania katika kuadhimisha siku hii muhimu ambayo inatupa fursa ya kujadili mambo mbalimbali yatakayoimarisha mahusiano yetu,”alisema.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Latifa Khamis alimshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwezesha biashara kufunguka.
Alisema Tanzania ni sehemu salama ya uwekezaji hivyo amewakaribisha wakorea kuja kufanya uwekezaji kwenye biashara mbalimbali nchini Tanzania.