Tanzania imeandika historia mpya ya matumizi ya rasilimali zake kufuatia kusainiwa kwa utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa chuma wenye thamani ya dola milioni 77, ambao utatekelezwa katika eneo la Maganga Matitu Wilayani Njombe unatarajiwa kuchochea maendeleo ya viwanda nchini na hivyo kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza Agosti 2, 2024 mkoani Njombe mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Uchimbaji Madini ya Chuma Maganga Matitu kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa NDC na Kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania .Co.Ltd. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema mafanikio hayo yametokana na jitihada za Serikali kuchochea matumizi sahihi ya rasilimali kwa manufaa ya Watanzania.

‘‘ Mhe. Rais amekuwa muumini wa kuikaribisha sekta binafsi iweze kushiriki kwenye uchumi wa nchi yetu ili tupate kodi na ajira kwa vijana wetu. Mradi huu na mingine mtaona dhamira yake ya kuona chuma kinachimbwa na kinapatikana,” amesema Dkt. Biteko.

Amesema, ‘‘ndio maana haikushangaza kulipa fidia bilioni 15 ili kupisha mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao ndio mradi mkubwa katika bara la Afrika tunaoutegemea. Nataka niwahakikishie watu wa Ludewa na Njombe mambo mengi zaidi yanakuja tuendelee kumuombea Rais Samia.”

Aidha, Dkt. Biteko ameongexa kuwa Serikali imekuwa ikijenga madaraja na miradi mingine mikubwa kwa kutumia chuma kutoka nje ya nchi ilihali kuna utajiri mkubwa wa chuma kwenye ardhi ya Tanzania.

Ametoa wito kwenye miradi mingine yote inayotekelezwa nchini na kusema kuwa Watanzania wanataka kuona rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao zinaleta maana kwenye maisha yao na kuwa utaratibu wa kuwa na rasilimali eneo fulani au kuchimbwa lakini sherehe za utiaji asaini mikataba au uzinduzi zinafanyika Dar es salaam au Dodoma kuwa si sawa ni lazima kwenda kwa wananchi wenyewe na kufanya jambo hilo kwa.

‘‘ Niwaombe wawekezaji muwe na hakika kuwa hakuna hasara mtakayopata katika kuwekeza Tanzania kwa sababu nchi yetu ina mazingira mazuri ya kibiashara na mahali tunapodhani kuna changamoto Mhe. Rais amekuwa akiunda kamati ili kurekebisha kasoro ndani ya mifumo ya Serikali, mtakumbuka kuna wakati haki jinai ilikuwa inalamikiwa na aliunda kamati na mapendekezo yake yanafanyiwa kazi na sasa ameunda tume ya kupitia malalamiko ya kodi, ’’amebainisha Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kufanya utafiti na kuwasilisha mapendekezo ya namna ya kufikisha umeme katika vijiji 10 vilivyopo pembezoni mwa Ziwa Nyasa eneo lenye milima wilayani Ludewa.

‘‘Nimekuja na wataalamu kutoka TANESCO na REA na nitaomba Mkuu wa Mkoa tupate mwakilishi kutoka Ludewa nataka tuunde timu ili tukapitie upya vijiji kisha tujadiliane na kukubaliana namna ya kufikisha umeme katika vijiji hivyo kama ni kwa kujenga njia kubwa ya umeme au kuweka gridi. Kazi ianze Jumatatu na ndani ya siku tano nipate majibu tujenge kwa namna gani.’’ Amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exhaud Kigahe amesema kuwa mwaka 2023, Rais Mhe. Dkt. Samia alilipa fidia ya takribani shilingi bilioni 15 kwa wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na mwaka 2020 aliahidi kutekelezwa kwa shughuli za uchumi ili maeneo yote ya uwekezaji yaweze kufanikiwa na sasa anamitiza ahadi yake.

Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolous Shombe amesema kuwa mradi huo wa kuzalisha chuma wa Maganga Matitu ni mradi mdogo ukilinganisha ule wa Mchuchuma na Liganga ambao tangu kuamuliwa kutekelezwa mwaka 2007 hadi kufikia hatua ya sasa ni takribani miaka 17.

Ameongeza ‘‘ Mradi huu utazalisha chuma ghafi ambacho kitatumiwa na vyuma vingine na hivyo tutakuwa na uchumi shindani kwa kuzalisha vyuma vitakavyotumika katika miradi mikubwa ya miundombinu. Katika mradi huu tunatarajia kuwekeza zaidi ya dola milioni 77.45 ambazo ni fedha za mtaji kutoka kwa mwekezaji na uzalishaji utaanza mwaka 2027, wananchi 385 watalipwa fidia kabla ya mwezi Januari ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni 4.25.’’

Vilevile, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania .Co.Ltd. Bw. Ix Xsinda amesema kuwa Kampuni yake imewekeza nchini kwa miaka nane na kuwa inamiliki kiwanda cha nondo kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema kuwa Mkoa wake utahakikisha unaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji watakaowekeza mkoani humo.

Rais Samia apata muarobaini mgogoro wa Wakulima, Wafugaji
SMZ yadhamiria kuleta mageuzi sekta ya Kilimo