Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa ametoa muda wa miezi miwili tu kwa uongozi wa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, kuhakikisha wanajenga vibanda vya wafanyiabishara wadogo wadogo maarufu kama machinga akielekeza kuwa agizo hilo ni kwa nchi nzima kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri.

Waziri Mchengerwa ametoa agizo hilo leo Agosti 3, 2024 mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake wilayani Mvomero alipozuru kwa ajili ya kuzungumza na wananchi na kuzindua kampeni ya miaka mitano ya Tutunzane Mvomero.

Akizungumza na maelfu ya wakazi wa Mvomero waliojitokeza kwa ajili ya kumsikiliza Rais, Waziri Mchengerwa amesema msingi wa makundi mengi ya wajasiriamali ni OR- TAMISEMI hivyo watendaji chini ya ofisi hiyo wanawajibika moja kwa moja kuhakikisha wanamaliza changamoto zinazoyakabili makundi hayo.

“Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kila mmoja wetu katika mipaka ya utawala wake hatuna budi kuhakikisha tunayalea makundi haya Pamoja na kuyaendeleza, kuyasikiliza na kuyasaidia pale ambapo yanapaswa kusaidiwa” alisema Mchengerwa.

Rais Dkt. Samia yuko ziarani Mkoani Morogoro ambapo anaendelea kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, kuzindua na kuweka jiwe la msingi, akitarajia kuhitimisha ziara yake Agosti 7, 2024.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Agosti 5, 2024
Dkt. Dugange: Tujitokeze kupiga kura uchaguzi Serikali za Mitaa