Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wawekezaji uwepo wa umeme wa uhakika katika Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga na hivyo amewaalika kwenda kuwekeza katika maeneo hayo.
Rais, Dkt. Samia ameyasema hayo Agosti 5, 2024 wakati akihitimisha ziara yake katika Mji wa Ifakara Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ambapo amesisitiza kuwa uongezaji thamani wa bidhaa katika viwanda unahitaji uwepo wa umeme wa uhakika hivyo Serikali inafanya kila jitihada ili nchi iweze kujitosheleza na nishati hiyo na kuwezesha uongezaji thamani malighafi zinazopatikana nchini ikiwemo mazao.
Amewahakikishia wawekezaji kuwa, maeneo ya Kilombero, Malinyi na Ulanga yatakuwa na umeme wa kutosha hivyo wawekezaji wasisite kuendelea kuwekeza katika viwanda mbalimbali.
Ameongeza kuwa, kupatikana kwa umeme katika maeneo hayo kumeendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani ambao wameweka mashine za kuchakata nafaka na kuongeza kuwa ujenzi mkubwa wa maghala unaendelea.
“Uwekezaji huu unaonesha kwamba umeme umeleta faida kubwa ndani ya maeneo haya, niwahakikishie Serikali itaendelea kusimamia Sekta ya Nishati ili kuendelea kuwa na umeme wa uhakika.” Amesisitiza Dkt.Samia
Akizungumzia miradi ya umeme vijijini, amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeshapeleka umeme kwenye vijiji vyote 110 vya Wilaya ya Kilombero.
Ameongeza kuwa kazi inayoendelea sasa ni upelekaji wa umeme kwenye Vitongoji na kwenye Taasisi.