Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kusimamia miradi ya maendeleo, ili kuondoa changamoto za kutokukamilika kwa miradi hiyo.
Sendiga ameyasema hayo mjini Babati wakati akifungua mafunzo kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata ambapo amebainisha kuwepo kwa changamoto zinazosababisha kutokamilika kwa miradi kutokana na usimamizi na ufuatiliaji hafifu.
Amesema, “tunakutana na changamoto nyingi za ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo ambayo hairidhishi katika maeneo mengi, tukikuta mradi una changamoto kwenye eneo lako basi Mtendaji wa Kata hapo umepwaya.”
Aidha, Sendiga amesema uwepo kwa changamoto hizo unaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi katika ngazi ya Kata na Tarafa zinazotokana na kutozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika utendaji kazi wa kila siku wa watendaji hao kama vile kuwepo kwa migogoro ya kiutendaji kati ya Wataalam hao na viongozi na Wataalam wengine katika ngazi hizo.
Changamoto nyingine ni pamoja na kutotatuliwa kwa wakati kero za wananchi na wadau wengine katika ngazi za msingi jambo linalosababisha wananchi kwenda kupata suluhu ngazi za juu ofisi ya Mkoa au Wilaya kwani zaidi ya asilimia 90 ya kero zinatokana na migogoro, kesi, malalamiko, ambazo Maafisa hao wanaweza kuzifanyia kazi na kushindwa kwao nao wanakuwa sehemu ya kero inayotakiwa kufanyiwa kazi.
Sendiga amesema Afisa Tarafa ndiye Msaidizi wa Mkuu wa Wilaya katika utekelezaji wa shughuli za Serikali Kuu katika Tarafa na Mtendaji wa Kata ni kiungo cha Uongozi kwa Idara zote kwenye Kata na hivyo Serikali inawategemea wao kama kiungo muhimu katika ngazi ya msingi.
Naye Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Beatrice Kimoleta amesema mafunzo hayo ya siku mbili yanatolewa na ofisi yake kupitia Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Regions and Local Government Strengthening Programme-RLGSP)
Aidha, amesema mafunzo haya yametolewa kwa awamu katika Mikoa 18 ya Tanzania Bara na hadi sasa mafunzo hayo yametolewa kwa washiriki 3,094 ambapo kati ya hao Maafisa Tarafa ni 340 na watendaji wa Kata 2,754 na katika awamu hii ya mwisho inahusisha mikoa nane ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya na Ruvuma ambapo Maafisa Tarafa 203 na Watendaji wa Kata 1,377 watapatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo.