Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -TAMISEMI, Festo Dugange amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo kufanya tathimini kwa haraka kupitia mapato yao ya ndani ili kufanya marekebisho kituo cha Mabasi cha Mbezi katika lango la kuingilia.

Dugange ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma wakati wa maswali na majibu wakati akijibu swali la Janeth Massaburi (Viti Maalumu) lililouliza Je, lini serikali itakamilisha ujenzi na miundombinu kwa asalimia 100 ya kituo kikuu cha Mabasi cha Magufuli – Mbezi.

Aidha, Dugange amesema kwa kutambua umuhimu na uhitaji wa kituo hiki cha mabasi kwa wamiliki wa mabasi, abiria na wafanyabiashara kwa mwaka 2024/25, serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imetenga shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya ukamilishaji wa kazi ambazo hazikukamilika ili kituo hiki kikamilike kwa asilimia 100.

Mradi huo ulikuwa ukijengwa na mkandarasi Hainan International LTD kwa mkataba kwa gharama ya shilingi bilioni 54.6 ambapo fedha toka ruzuku ya serikali kuu ni shilingi 50.9 na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Ubungo shilingi bilioni 3.6.

“Hadi kufikia mwezi Agosti 2024 jumla ya shilingi bilioni 49.8 zimetumika katika kutekeleza mradi huo na umefikia asilimia 97 aidha baadhi ya kazi zilipangwa kutekelezwa zimekamilika na nyingine zipo hatua mbalimbali za ujenzi kama ujenzi wa basement 1&2, ujenzi wa ghorofa ya tatu eneo la abiria na ujenzi wa eneo la kuingilia magari,” amesema Dugange.

Amesema katika mwaka 2023/24, serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imelipa shilingi milioni 545 na shilingi bilioni 1.6 zipo kwenye utaratibu wa kumlipa mkandarasi ili kuendelea na ujenzi.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Septemba 2, 2024
Wataalam Tiba Asili watakiwa kufikiri kisayansi