Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameongeza adhabu ya faini kutoka shilingi milioni 3 hadi milioni 5 kwa msanii Seif Kisauji maarufu (Babu wa TikTok) na kumtaka aombe msamaha hadharani kutokana na kosa la kurusha maudhui ya sanaa yanayokiuka maadili mtandaoni.

Waziri Ndumbaro ametoa uamuzi huo hii leo Septemba 4, 2024 Mtumba Jijini Dodoma baada ya kusikiliza rufaa ya msanii huyo ya kupinga adhabu aliyopewa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ya kufungiwa kujihusisha na shughuli za sanaa kwa miezi 6 pamoja na kulipa faini ya shilingi milioni 3 kutokana na kurusha mtandaoni picha za video zinazokiuka maadili.

Aidha, kufuatia rufaa hiyo, msanii Seif Kisauji amekiri kosa la kusambaza maudhui hayo na kuomba apunguziwe adhabu hatua iliyomfanya Waziri Dkt. Damas Ndumbaro amuondolee adhabu ya kifungo cha cha miezi 6 cha kutojihusisha na shughuli za sanaa huku akimuongezea kiwango cha faini kutoka milioni 3 hadi 5.

“Sheria ya BASATA iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kifungu cha 15 A inampa mamlaka Waziri kusikiliza rufaa na kutoa maamuzi, hivyo kwa kushauriana na Naibu Waziri, Hamis Mwinjuma ambaye ndiye msimamizi wa sekta ya sanaa, nimefuta adhabu ya miezi sita aliyopewa kuanzia leo, na ninamtaka azingatie maadili katika kufanya kazi zake” amesisitiza Ndumbaro.

Awali, katika kikao hicho Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamis Mwinjuma alimtaka Msanii huyo, kurudi katika sanaa aliyokua akiifanya zamani ambayo ndiyo iliyomfanya jamii imtambue na kuelewa kuwa yeye ni kioo cha jamii hivyo anapaswa kufanya Sanaa inayoelimisha na kuburushisha jamii bila kuharibu mila na desturi za Kitanzania.

Kwa upande wake Msanii Seif Kisauji ameishukuru wWizara kukubali rufaa yake pamoja na kuridhia msamaha na kumfungulia kufanya sanaa akiahidi kujirekebisha na kufanya sanaa zenye maadili na kuwa Balozi mzuri kwa wasanii wenzake.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Septemba 4, 2024
Wananchi, Viongozi wahimizwa tahadhari ya Mpox