Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limekemea matukio ya kikatili dhidi ya Watoto na Wanawake yanayohusisha vitendo vya kulawiti na kubaka ambavyo wakati mwingine yanapelekea wahanga kupoteza maisha.

Katika hatua hiyo, Septemba 3, 2024 pia imefanya kikao na Waganga wa tiba mbadala 80 kwa lengo la kuwaelemisha kuacha kujihusisha au kufanya ramli chonganishi, ikiwa na pamoja kuacha tabia ya kuwapa masharti baadhi ya wateja wao kuwa ili wafanikiwe kwenye biashara na kupata utajiri lazima wafanye vitendo viovu vya kuwalawiti au kuwabaka watoto wadogo.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne imeleeza kuwa katika kusimamia mifumo ya kisheria na utekelezaji wa taarifa ya tume ya haki jinai, Polisi imeendelea kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya kihalifu ambao baadhi yao wamepatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kupewa adhabu.

Amesema, washtakiwa katika kesi 16 kuanzia za makosa ya kubaka na kulawiti zilizo sikilizwa kati ya Julai hadi Agosti 2024 walihukumiwa adhabu za vifungo akiwemo Boniphace Paul @ devi (24) mkazi wa Mbezi kwa Msuguli, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, shauri la jinai No. 192/2023 mbele ya Hakimu Mkazi Amos Rweikiza kwa kosa la kumbaka na kulawiti Mwanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 13 ambapo baada ya shauri lake kusikilizwa Agosti 15, 2024 mshtakiwa alipatikana na hatia na kuhukumiwa na kufungwa kifungo cha maisha jela.

Aidha, Mshtakiwa George Godfrey (21) Mkazi wa Chanika naye alimakatwa maeneo ya Coco Beach na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia Silaha ambapo baada ya shauri lake kusikilizwa tarehe Agosti 28, 2024 alipatikana na hatia na kuhukumiwa na kufungwa kifungo cha miaka 30 jela.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Septemba 3, 2024 majira ya saa mbili (2) usiku, lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa maeneo ya Kawe Tanganyika Packers kulikuwa na watu wawili waliokuwa na mapanga huku wakitishia na wanawapora wapita njia.

Ufuatiliaji wa Polisi ulifanyika haraka na kuwakuta watu hao, walipotaka kukakamtwa walikaidi na kutoa mapanga kutaka kumdhuru mmoja wa askari, ambaye alijihami kwa kupiga risasi hewani na baadae alipokuwa kwenye hatari kubwa ya kudhuriwa alimjeruhi kwa risasi mtuhumiwa mmoja Festo Maricha (27) mkurya, Mkazi wa Mbezi Luis na mwenzake ambaye hakufahamika jina alikimbia.

Mtuhumiwa amepelekwa Hospitali ya Mwanayamala kwa matibabu ambapo Polisi linatoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali zitazosaidia mkakati wa kuzuia zaidi vitendo vya kihalifu ili Jiji la Dar es Salaam liendelee kuwa salama.

Babati waanza Uboreshaji Daftari la kudumu la wapiga kura
Wakandarasi Wazawa wababaishaji wanyoshewa kidole