Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeenda Tamasha la tatu la Utamaduni la Kitaifa, ambalo litafanyika Mkoani Ruvuma, katika manispaa ya Songea kuanzia tarehe 20 hadi 23, Septemba 2024.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dodoma katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gerson Msigwa ambapo amesema tamasha hilo litafunguliwa na Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Septemba 20, 2024.

“Aidha kilele cha tamasha hili ni tarehe 23 Septemba, 2024, mgeni rasmi ambae atafunga tamasha hilo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan”, amesema

Na tamasha hili limebeba Kaulimbiu
isemayo ‘’Utamaduni wetu ni utu wetu, tuuenzi na kuuendeleza, Kazi iendelee’’ , hili tamasha limekuwa na faida nyingi kwa jamii ambazo ni pamoja na kuenzi utamaduni wetu, kuimarisha ushikamano wa kitaifa, kuitangaza nchi yetu, kutangaza vivutio vya kiutalii na kiutamaduni, fursa za kiuchumi, na kijamii, kutanua wigo na mitandao ya kibiashara kwa bidhaa zinazozalishwa nchini hususani bidhaa za utamaduni, sanaa, na ubunifu”. Amesema Msigwa

Madhumuni ya tamasha hili ni pamoja na kuenzi na kulinda utamaduni wetu, kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia ukuzaji wa sekta za ubunifu na utamaduni, kutoa jukwaa la kuonyesha utamaduni kama msukumo madhubuti wa utangamano wa kitaifa kwa kuwaleta na kuwaunganisha pamoja wadau na viongozi wa sekta, kuendeleza na kuenzi urithi wa utamaduni wetu, kutoa fursa ya majadiliano ya kitaaluma baina ya wananchi wa kila mkoa, kutumia utamaduni na ubunifu kama nyenzo ya kuenzi na kukuza utambulisho wa Taifa na kutangaza fursa na rasilimali za kipekee ilizonazo nchi yetu”,amesema

Tamasha la mwaka huu litakuwa na vionjo mahususi kama mirindimo ya kiasili, kuanzia mavazi, maonesho, visasili na visakale, litakuwa na mdahalo wa kitaifa utakaozungumzia mapambano dhidi ya viashiria vya mmomonyoko wa maadili na nini mchango wa jamii katika kupunguza na hatimaye kuondoa viashirika hivyo, litakuwa na onesho maalumu la matumizi ya kanga ikiwa ni vazi la utamaduni wa Mtanzania, litakuwa na zaidi ya vikundi 25 kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar; vikundi hivyo ni vya sanaa ya asili, ubunifu, utamaduni na mziki wa kizazi kipya, litakuwa na mashindano ya uhifadhi wa ngoma za asili kwa vikundi 25 vya Tanzania Bara na visiwani, litakuwa na kliniki ya Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo”. Amesema Msigwa

Amesema Kutokana na umuhimu na mvuto wa tamasha hili, ameziomba kampuni zote, mashirika, asasi na taasisi zinazotoa huduma mbalimbali, washirika wa maendeleo na wadau kwa ujumla kujitokeza kudhamini tamasha hilo.

Ameongezea kwa kusema , tamasha hilo ni fursa muhimu katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisayansi, kisiasa na kiutamaduni. Aidha, ni njia mahususi ya kukuza viwanda vya ubunifu sanaa na utamaduni nchini.

Yanga kuilipa Azam shilingi milioni 88.5
Kagera: Maafisa ugani warahisishiwa utendaji kazi