Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa ameuelekeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa bwalo la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Sayansi ya Mkoa (Longido Samia Girls) ifikapo Novemba mosi, 2024.

Akizungumza wakati alipotembelea shule hiyo, Waziri Mchengerwa amesema dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni wanafunzi wake wapate chakula kwenye Bwalo.

“Serikali imeshaletewa fedha zote kwa ajili ya ukamilishaji wa Bwalo la chakula kwa wanafunzi lakini mpaka sasa bwalo halijakamilika watoto wanapata shida wakati wa wanakula chakula, Rais Samia anataka wanafunzi wake wale kwenye Bwalo na sio kama wanavyoteseka kwa sasa,” amesema.

Amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Longido kuhakikisha anasimamia ujenzi huo na mafundi wafanye kazi usiku na mchana kwa ubora na kuzingatia thamani ya fedha.

Aidha, Mchengerwa amesisitiza uwekaji wa miundombinu ya Nishati Safi ya kupikia ili shule hiyo iweze kutumia Nishati hiyo kupikia na kuachana na kuni banifu au mkaa ambao una athari kwa afya ya binadamu.

Shule hiyi inajengwa kupitia mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na imekwishapokea sh. Bilioni 4.1 kwa ajili ya majengo yote yanayohitajika na hadi sasa ina wanafunzi zaidi ya 170 wanaoendelea na masomo ya kidato cha tano.

Kagera: Vitongoji 135 kunufaika Mradi Umeme wa REA
Taasisi za dini zishirikiane kukemea maovu - Dkt. Mwinyi