Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, linawashikilia Wafanyakazi wa Kampuni ya mikopo ya OYA kwa tuhuma za mauaji ya Juma Said Mfaume kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili ambaye alikuwa ni mume wa mdaiwa wao, Khadija Ramadhani huko Mlandizi, Kibaha Mkoani Pwani.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Muhudhwari Msuya amesema tukio limetokea Oktoba 7, 2024 katika kitongoji cha Mbagala Wilaya ya Kipolisi Mlandizi ambapo Wafanyakazi hao walifika nyumbani hapo kwa lengo la kudai fedha za marejesho ya mkopo kwa mke wa marehemu.

Amesema, baada ya kufika nyumbani kwa Juma aliwaelekeza kuwa mkewe hayupo lakini watuhumiwa hao walilazimisha kuingia ndani kwa nguvu huku wakimshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo kisha alianguka chini na kupoteza fahamu.

Amesema, kutokana na hali hiyo Watuhumiwa walimbeba Juma kwenye gari lao kumpeleka Hospitalini lakini alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha afya cha Mlandizi.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linatoa wito kwa makampuni na taasisi za kifedha kufuata taratibu za kisheria katika kudai fedha kutoka kwa wateja wao, ili kuepusha usumbufu na madhara yanayoweza kutoka ikiwemo uharibifu wa Mali, kujeruhi na vifo.

Ziara ya Kikazi: Waziri wa Mambo ya Nje awasili Finland
Mbagala: NEMC watekeleza agizo la Waziri Mkuu