Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi (Na.13)wa Mwaka 2024, kama ulivyowasilishwa unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura ya 366 (The Employment and Labour Relations Act, Cap, Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300 (The Labour Institutions Act, Cap. 300) na Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436. The Non-Citizen (Employment Regulation) Act, Cap. 436).
Naibu Waziri wa Nchi – Ofisi Ya Waziri Mkuu kazi, Vijana, ajira na wenye Ulemevu, Patrobas Katambi ameyasema hayo wakati akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Za Kazi (na.13) wa Mwaka 2024 Bungeni jijini Dodoma.
“Mheshimiwa Spika, Muswada huu umegawanyika katika Sehemu Nne, Sehemu ya Kwanza inahusu masharti ya utangulizi ambayo yanajumuisha jina la Muswada na namna ambavyo masharti ya Sheria mbalimbali yanapendekezwa kurekebishwa”,amesema
“Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Pili ya Muswada inapendekeza marekebisho kwenye
Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini,
Sura ya 366 ambapo kifungu cha 4 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuboresha na kuongeza tafsiri ya baadhi ya misamiati iliyotumika katika Sheria,” amesema Katambi
Amesema Lengo la marekebisho hayo ni kutoa fafanuzi wa matumizi ya misamiati hiyo ambayo imetumika katika Sheria.
“Kifungu cha 9 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuongeza wigo wa tafsiri ya msamiati “senior management employee”, Lengo la marekebisho haya ni kuongeza wigo wa ufafanuzi wa nafasi ya mfanyakazi mwandamizi katika menejimenti kwenye utekelezaji wa haki ya kujiunga katika vyama vya wafanyakazi”,amesema
“Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 14 kinapendekezwa kurekebishwa ili kubainisha aina ya mikataba ya muda maalum, lengo la marekebisho haya ni kuongeza wigo wa mazingira ambayo mtu anaweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi maalum, ikiwemo mikataba ambayo mwajiriwa anaajiriwa kwa muda ili kuendana na ongezeko la wingi wa kazi, kutoa fursa kwa wahitimu wa vyuo ili kuwajengea uwezo na kufanya kazi nyingine
za misimu”.Amesema Katambi
Amesema, Kifungu kipya cha 16A kinapendekezwa kuongezwa ili kubainisha mazingira ambayo mwajiri na mwajiriwa wanaweza kuingia katika makubaliano ya namna watakavyofanya kazi katika hali ya dharura inayoweza kuathiri uzalishaji mahali pa kazi.
“Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha ulinzi wa ajira na usalama wa
manyakazi mahali pa kazi, kuwezesha uzalishaji na kupunguza athari kwa waajiri wakati wa magonjwa ya milipuko na matukio ya dharura.”
“Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 33 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti kwa kujumuisha katika likizo yake ya uzazi muda uliobaki kufikia wiki arobaini za ujauzito. Lengo la marekebisho haya ni kulinda ustawi na afya za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ambao wanahitaji muda wa kutosha wa uangalizi wa mama”. Amesema Katambi
Awali, katika Muswada ilipendekezwa muda wa wiki thelathini na sita za ujauzito kama ukomo wa muda wa mtoto kutimia.
“Hata hivyo, baada ya majadiliano na Kamati, Serikali ilikubaliana na mapendekezo ya kongezwa muda huo hadi kufikia wiki arobaini. Vilevile, Serikali ilikubaliana na pendekezo la Kamati la kongeza muda wa likizo ya Baba ambaye atapata mtoto njiti, ambapo, badala ya likizo ya muda wa kawaida wa siku 3 atapata siku saba”
“Mapendekezo haya yamejumuishwa katika Jedwali la Marekebisho la Serikali. Kifungu kipya cha 34A kinapendekezwa kuongezwa ili kumwezesha mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku thelathini. Lengo la marekebisho haya ni kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mwajiriwa kupata likizo bila vikwazo,” amesema Katambi