Eunice Kanumba – Shinyanga.  

Vijana wasomi Mkoani Mwanza, wametakiwa kuiga mfano wa Vijana walioko katika mpango Jenga Kesho yako Bora (BBT), Wilayani Kishapu ambao waliamua kujitolea na kuitumia elimu ya Kilimo ya Chuo Kikuu waliyopata kulima mashamba ya mfano, wakilenga kuchochea ari kwa Wakulima, ili waweze kuzalisha kwa ufanisi.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha katika ziara yake ya kukagua na kuhamasisha kilimo cha zao la Pamba Kata ya Ngofila Wilayani Kishapu, ambapo ametembelea vijiji vinavyozalishaji zao hilo vya Mwamanota, Idushi na Ngofila na kukutana na vijana hao ikiwa ni sehemu yao ya kujiajiri na hivyo kuwa sehemu ya mfano na chachu kwa vijana wengine.

Amesema, “miwashauri vijana na wasomi wetu mkoani Shinyanga, njooni muige na kujifunza namna bora ya kujiajiri na kutumia vema nguvu, elimu na maarifa mliyonayo huku Kata ya Ngofila wilayani Kishapu ambapo kuna vijana wenzenu kutoka kundi la Jenga Kesho iliyo Bora ambao wameamua kujitolea na kutumia elimu, maarifa na muda wao kuwasaidia wakulima katika kilimo cha pamba na wao pia kulima mashamba ya mfano ikiwa sehemu ya kujiajiri na kuongeza pato binafsi.”

RC Macha amesema, katika utekelezaji wa majukumu yake  kwa sasa atakuwa anapatikana zaidi  maeneo ya vijijini ambako ndipo walipo wakulima na kwamba atatumia muda mwingi zaidi kuhamasisha na kuwatia moyo wakulima wote ili kuhakikisha heshima na hadhi ya zao la  pamba mkoani Shinyanga inarejea kama ilivyokuwa hapo awali, kwani pamba (dhahabu nyeupe) ni sehemu ya utambulisho wa Mkoa wa Shinyanga.

Ametolea mfano wa shamba la Mkulima wa Kijiji cha Ngofila, Raphael Zengi ambaye msimu wa 2023/2024 alipata kilo 4605 kwa hekari nne ambao ni wastani wa kilo 1150 kwa hekari moja, na kusema huo ni mlengo na nia ya Serikali ya kuhakikisha kila Mkulima anapata kuanzia kilo 1000 au zaidi kwa hekari moja.

Aidha, kwa upande wake Raphael alisema anatarajia kuvuna kilo zaidi ya 1200 kwa kila hekari moja msimu huu wa 2024/2025 kwa kuwa ameboresha, amezingatia maelekezo ya wataalam na ameongeza eneo la kilimo chake, huku akiishukuru serikali  kwa kuwawezssha kupata pembejeo zote muhimu tena kwa wakati jambo ambalo limewatia moyo na hamasa ya kulima zaidi pamba msimu huu.

Awali, akitoa salamu za Wilaya kwa mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kishapu,  Peter Masindi amesema  kuwa kwa ujumla wakulima wanayo ari, nguvu na hamasa kubwa ya kulima na kwamba ujio wake utaongeza morari   zaidi ya kulima ili mwisho wa siku lengo la kuongeza kipato kwao, kuimarisha uchumi na pato la Taifa liweze kufikiwa kwa pamoja.

Naye afisa kilimo Kata ya Ngofila, Mathias Nyanda amesema Kata hiyo yenye kaya 1619 na Vijiji 5 ambavyo ni Ngofila, Kalitu, Inolelo, Mwamanota na Idushi pamoja na kilimo cha pamba, pia Wananchi wake wanajishughulisha na Kilimo cha Mahindi, Choroko, Mtama, Dengu, Alizeti, Mpunga na Viazi vitamu huku Pamba pekee ikiwa imelimwa takribani ekari 25,000.

Kamati ya Bunge yapongeza uwekezaji wenye tija
Maisha: Kwa tukio hili, nimeamini kweli uchawi upo