Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma amesema hadi  kufikia mwezi Machi 2025, jumla ya leseni 206 za Televisheni na Redio za mtandaoni zimetolewa. Mwinjuma ameyasema hayo leo Aprili 8,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mpendae Toufiq Turky aliyehoji Serikali imejipangaje kuhakikisha ongezeko la vyombo vya habari mtandaoni haliathiri maadili na utamaduni wa Taifa. “Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kutoa leseni za vyombo vya habari na waandaaji wa maudhui mtandaoni kwa maombi ambayo yanakidhi vigezo vilivyowekwa ili kupanua wigo wa kutoa habari nchini kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Utangazaji,” amesema.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali kupitia TCRA imeendelea kutoa elimu na imekuwa na programu maalumu za kuwaelimisha watumiaji wa mitandao kuhusu matumizi sahihi na salama ya mitandao na kuendelea kufuatiilia wale wanaokiuka maadili ya mtanzania na kuwawajibisha ikiwemo kuwafungia uzalishaji wa maudhui na kuwapiga faini kwa mujibu wa sheria za vyombo vya habari na za nchi. “Serikali imeanzisha Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Bodi hiyo inasimamia weledi na maadili kwa waandishi na kuhakikisha waandishi wenye sifa ndio wanaoruhusiwa kutumika katika vyombo vya habari.”

RSA watoa somo uhalisia wa majina ya Barabara, umbali
BUNGENI: Matemanga wanapata Majisafi na Salama - Mha. Kundo