Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema shule mpya ya wavulana kidato cha tano na sita itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 300, na itajumuisha mabweni, maktaba ya kisasa, bwalo kubwa la chakula, viwanja vya michezo pamoja na nyumba za walimu.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, ambapo amewaongoza Mawaziri, Wabunge na Wananchi katika mbio za hisani za Bunge Marathon 2025, zilizoandaliwa kwa lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Bunge ya Wavulana ya kidato cha tano na sita.

“Ujenzi wa shule hiyo itakayokuwa na uwezo wa kusajili wanafunzi wasiopungua 300 hadi 350 kwa mwaka utagharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu,”ameeleza Majaliwa
Shule hiyo ya kidato cha tano na sita itajengwa katika eneo la Kikombo, Jijini Dodoma karibu kidogo na shule ya wasichana iliyojengwa na wabunge wanawake 2020”, amesema

“Ninawapongeza sana Wabunge wenzangu kwa kuweka alama na kugusa maisha ya Watanzania na watoto wetu wa kiume watakaopata fursa ya kusoma katika shule hiyo,” amesema Majaliwa

Amesema ujenzi wa shule hiyo ni mpango wa Bunge wa kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia suluhu Hassan katika kukuza na kuendeleza sekta ya elimu.

“Shule hiyo ya bweni itakuwa na maabara nne za biolojia, kemia, fizikia na jiografia, maktaba, bwalo la chakula, nyumba za walimu pamoja na viwanja vya michezo,” amesema.

Hata hivyo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, alisema kuwa baada ya mafanikio ya ujenzi wa Shule ya Bunge ya Wasichana, sasa Bunge linaendelea na ujenzi wa shule ya wavulana kama ishara ya kuonesha usawa wa kijinsia na dhamira ya kuwatunza na kuwaendeleza watoto wote wa Tanzania bila ubaguzi.

“Mbio hizi za hisani pia zimetoa fursa kwa washiriki kujenga afya zao na kuungana kwa pamoja katika azma ya kulijenga taifa kupitia elimu,” amesema.

“Bunge limeona umuhimu wa kujenga shule ya sekondari ya wavulana, na hii ni baada ya kuwa na shule ya Bunge ya wasichana, Watoto wote ni wetu, na ndio maana tukaona umuhimu wa hili. Nawashukuru washiriki wote kwa mchango wao katika ujenzi huu,” amesema Dkt. Tulia.

Vilevile Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Bunge Marathon 2025, Mheshimiwa Festo Sanga, amesema mbio za mwaka huu zimevutia washiriki zaidi ya elfu 4, ongezeko kubwa kutoka washiriki elfu 3 wa mwaka 2024, jambo ambalo linaonesha jinsi ambavyo wananchi wanazidi kuhamasika kushiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo kupitia Bunge Marathon.

Ajali yachukua uhai wa Mkurugenzi wa TANESCO
Oltorok wavunja ukimya ujenzi wa Zahanati, RC Sendiga atoa maagizo