Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden amemtaka Rais mteule wa Marekani Donald Trump kukomaa kiakili na kufanya mambo ya kikubwa kuendana na hazi yake ya urais huku akamshutumu kwa kukosoa majasusi wa Marekani.
Biden amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kwa rais mteule kutokuwa na imani na mashirika ya kijasusi ya nchi yake ambayo yanashughulikia masuala ya usalama
“Kwa rais kutokuwa na imani na kutokuwa tayari kuyasikiliza mashirika ya ujasusi, kuanzia majasusi wa jeshi hadi majasusi wa CIA, ni jambo la kukosa hekima kabisa,” amesema Biden.
Aidha, Biden amemtaka Donald Trump kukomaa na kusema kuwa wakati wa kukomaa na kuwa mtu mzima umefika kwani yeye ni rais wa taifa kubwa na lenye nguvu duniani.
Hata hivyo, Biden amesema ameshasoma ripoti ya mashirika ya ujasusi ya Marekani ambayo inaonyesha wazi kuwa Urusi ilihusika katika udukuzi kadiri uchaguzi ulivyokaribia.
Akizungumzia ripoti hiyo, Biden amesema ripoti hiyo inaeleza wazi walichofanya Warusi kama sehemu ya sera yao kujaribu kuathiri na kutia doa shughuli za uchaguzi Marekani.