Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umewataka watendaji na watumishi wa Makao Makuu ya jumuiya hiyo kuanza kujipima, kujitathmini na kujipanga upya kimkakati kwa sababu muda wa kupiga maneno haupo ila vinavyohitajika ni uwezo binafsi na vitendo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka amesema hayoa alipokutana na kufanya kikao na watumishi wa UVCCM Makao Makuu kwa ajili ya kutathmini utendaji wa jumuiya kwa mwaka 2016 na kupanga mikakati ya utekelezaji wa majukumu kwa mwaka 2017.
Shaka amesema kuwa pamoja na kusikiliza michango , maoni , ushauri , mawazo na changamoto zinazowakabili watumishi na namna ya kuzitatua kwa mwaka 2017 lazima uwe mwaka wa vitendo na mafanikio.
“Tutabadili kila kona yenye kasoro au dosari , lengo si kukomoana ila ni katika kujipanga tena upya, asiyeweza aseme hawezi ili akae kando , kama mtu hajimudu hatapewa dhamana yoyote kwasababu ya ushikaji na urafiki “Amesema Shaka.
Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo amesema makao makuu inahitaji kuwa kama kioo, sifa ya kioo ni kujiona na kujitambua, kama umechafuka jisafishe ili uwe nadhifu na makini bila mtu kusukumwa.
Hata hivyo Shaka amewataka wana jumuiya mahali popote walipo nchini wajione na kujihesabu wao ni ndugu wa tumbo moja, wapendane, wasikubali kukaribisha majungu au hasama kwasababu zama hizo zimepita na hazitarejea tena.