Imezoeleka kuwa shabiki ndiye ‘Bosi’ wa msanii, lakini Mwana FA anaamini Bosi huyu hapaswi kuwa muamuzi wa anachopaswa kufanya msanii huyu.
Mkali huyo wa ‘Dume Suruali’ ametaja kile anachokiita kosa kubwa ambalo hufanywa na wanamuziki wengi nchini kuwapa nafasi mashabiki kuyumbisha msimamo wa muziki wao.
“Nadhani kosa wanalofanya wasanii wengi ni kuwaacha mashabiki wau-control muziki wako. Yaani mashabiki ukiwaacha wakuamlie ufanye muziki gani, mara siku hizi umebadilika… mimi napaswa nifanye muziki ninaoutaka halafu wewe ndio uamue kuupenda au kutoupenda muziki wangu,” alisema Binamu kwenye ‘The One Show ya TV1.
Katika hatua nyingine, Mwana FA alieleza kuwa pamoja na changamoto nyingi zinazojitokeza, teknolojia na mitandao imesaidia kurahisisha usambazaji wa muziki duniani tofauti na enzi zile ambazo msanii aliyekuwa Dar alipaswa kwenda Ubungo kutuma CD yake Mwanza.
FA ni mmoja kati ya waliouaga vyema mwaka 2016 na kuukaribisha kwa tabasamu la pesa mwaka 2017 baada ya wimbo wake ‘Dume Suruali’ kuvunja rekodi ya nyimbo zake zote kwenye mtandao wa YouTube huku ikiiteka mitaa na vyombo vya habari.