Serikali imesema kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha na kuwataka wananchi kupuuza taarifa zinazodai kuwa hali ya chakula ni mbaya.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam kuhusu hali ya upatikanaji na chakula nchini.
“Ndugu waandishi ukweli ni kwamba hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha sana katika maeneo mengi, hivyo siyo kweli kwamba kuna tatizo la njaa kama baadhi ya watu wanavyojaribu kupotosha,” amesema Dkt. Tizeba.
Aidha Dkt. Tizeba aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa hali nzuri ya chakula, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea kuweka akiba ya chakula kwa kununua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na chakula cha kutosha.
Dkt. Tizeba amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imejipanga kununua jumla ya tani 100,000 za chakula ambapo hadi kufikia Januari 8 mwaka 2017 imenunua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo ililojiwekea.
“Kati ya kiasi kilichonunuliwa, tani 38,162.280 zimenunuliwa kupitia vituo vya ununuzi na tani 23,925.717 kupitia vikundi vya wakulima hivyo hadi kufikia tarehe 12 Januari, 2017 Wakala wana akiba ya tani 88,152.443 za mahindi,” alisema Dkt. Tizeba.
Hata hivyo, Tizeba ameongeza kuwa hadi kufikia katikati ya mwezi Januari, 2017 hali ya chakula na upatikanaji wake hapa nchini bado ni ya kuridhisha na hasa upatikanaji wa vyakula kama mchele na maharage ikilinganishwa na zao la mahindi.