Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Moses  Nnauye, amewataka wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kufanya kazi kwa ari ili kuhakikisha linakuwa mfano Barani Afrika  katika kuhabarisha umma.

Nape ameyasema hayo mapema hii leo  alipofanya ziara katika Shirika hilo ili kuona utendaji kazi pamoja na kuona  changamoto mbalimbali  zinazolikabili Shirika hilo.

“Fanyeni kazi kwa bidii na uadilifu kwa kutoa taarifa za ukweli na zenye uhakika kwa watazamaji puuzeni  propaganda zinazoenezwa mtaani kuwa Shirika hili limepoteza Watazamaji na wasikilizaji kwa manufaa ya Taifa letu”.Amesema Waziri Nape.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dkt.Ayoub Ryoba amesema kuwa  Shirika linaendelea kuongeza wasikilizaji na watazamaji   ambapo kuanzia mwaka 2012 hadi 2016 limeongeza mitambo kutoka  kumi na mbili hadi hadi kumi na tisa  iliyofungwa   Mtwara,Rombo,Mbambabei na Tarime.

Aidha, Dkt Ryoba ameongeza kuwa  Shirika hilo  bado linaendelea  kuwa katika historia  ya Kuwa Shirika lililohabarisha umma juu ya Jitihada za Serikali ya Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika pamoja na   kuendelea kukuza lugha ya Kiswahili kupitia kipindi cha malenga wapya.

“Shirika  letu linaendelea kutoa habari, elimu na burudani zinazozingatia muktadha wa Utamaduni wa Nchi yetu  ambapo kwa kipindi cha mwaka jana tumekuwa tukirusha matukio  mubashara kupitia mitandao   ambayo yana  wafuatiliaji zaidi ya million tano.” Alisema Dkt.Ryoba.

Shirika hilo linaendelea kuwafikia watazamaji na wasikilizaji wengi zaidi ndani na nje ya nchi kwa kuendelea kuweka mikakati ya  kuongeza vituo vingi zaidi

Video: Nchi haijakumbwa na baa la njaa - Majaliwa
Waziri Tizeba awatoa hofu watanzania kuhusu chakula