Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda lililogharimu shilingi milioni 55 litakalohudumia mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Tabora na litatoa huduma kwa vituo vya kutolea huduma za afya 580 ikiwa ni pamoja na hospitali za rufaa za mikoa miwili ya Kigoma na Tabora, Hospitali za wilaya sita za Nzega, Igunga, Urambo, Kobondo, Kasulu na Mpanda Mji.
Majaliwa amefungua duka hilo lililoko katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi leo Januari 17, 2017 ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa MSD Agosti 20, 2016 alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Katavi. Aliuagiuza uongozi MSD kujenga duka hilo ili kurahisisha upatikanaji wa dawa katika mkoa huo pamoja na mikoa jirani.
Majaliwa amesema baada ya kufunguliwa kwa duka hilo Serikali haitarajii kusikia tena katika vituo vya afya na Zahanati zilizoko mkoani Katavi na mikoa jirani zinakosa dawa. Amewaagiza Wakurugenzi kusimamia suala hilo na kuhakikisha vituo vyote vya afya vinakuwa na dawa za kutosha.
Aidha, ameziagiza Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kukutana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kutafuta namna bora ya kutumia fedha za huduma za afya zinazipatikana katika halmashauri nchini.
Aamesema Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Katavi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.