Vinara wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Wekundu Wa Msimbazi Simba leo watajaribu kusogea mbali na wapinzani wao wakuu katika mbio za ubingwa msimu wa 2016/17, Young Africans.
Simba SC watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar katika mchezo wa mzunguuko wa 19 wa ligi kuu Uwanja wa Jamhuri, Mjini Morogoro.
Na baada ya Young Africans kushinda bao moja kwa sifuri dhidi ya Maji Maji Uwanja wa Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma hapo jana, iliikaribia Simba kwa tofauti ya moja kutoka nne.
Simba leo watakuwa na jukumu la kupigania ushindi ili kurudisha gepu la pointi nne na kendelea kuongoza vizuri mbio za ubingwa wa Ligi Kuu wakiwaacha mbali mabingwa hao watetezi.
Lakini hilo halitarajiwi kuwa jepesi kutokana na hali halisi ya kikosi cha Mtibwa Sugar kwa sasa na dhamira yao ya kutotaka kupoteza mchezo pamoja na historia ya mechi za timu hizo, huwa kali na zisizotabirika.
Tayari Mtibwa Sugar kupitia kwa msemaji wao Thobias Kifaru wamekwishasema kwamba; “Simba hawatoki Jamhuri”.
Lakini upande wa Simba napo, chini ya Kocha Mkuu, Mcameroon Joseph Marius Omog dhamira yao ni kucheza kila mchezo kama fainali kuhakikisha wanashinda.
Omog anaamini Simba inakamiwa katika kila mchezo na ili kushinda ni lazima kucheza kama fainali kwa kupigana kwa nguvu zote mwanzo mwisho.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo unatarajiwa kufanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kati ya wenyeji, Azam FC dhidi ya Mbeya City.