Mshambuliaji kutoka nchini Uholanzi Memphis Depay amekubaliana maslahi binafsi na uongozi wa klabu ya Olympic Lyon, ikiwa ni sehemu ya uhamisho wake wa kuondoka nchini England na kuelekea Ufaransa katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Taarifa kutoka mjini Lyon zinaeleza kuwa, Depay yu njiani kuondoka Old Trafford kuafuatia mambo kumuendea kombo tangu Jose Mourinho alipowasili klabuni hapo mwanzoni mwa msimu huu.

Uongozi wa Man Utd nao umeripotiwa kuwa katika mazungumzo ya mwisho ya kukamilisha biashara ya kumuuza Depay ambaye alijiunga na mashetani hao mwaka 2015 akitokea nchini kwao Uholanzi alipokua akiitumikia PSV Eindhoven.

Hata hivyo mpaka sasa, pande hizo mbili hazijafikia makubaliano ya kiasi cha pesa ambacho kitatumika kama ada ya usajili wa Depay, kufuati uongozi wa Olympic Lyon kuhitaji ishuke kutoka Pauni milion1 13 hadi milioni 11.

Meneja wa Olympic Lyon Bruno Genesio amekua chachu ya kuushurutisha uongozi wa juu wa klabu hiyo, kuhakikisha usajili wa muholanzi huyo unakamilika katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Genesio anaamini endapo atafanikiwa kumsajili Depay, atakuwa amekisaidia kikosi chake kumpata mtu ambaye atasaidia katika safu ya ushambuliaji, ili kutimiza malengo waliojiwekea kwa msimu huu wa 2016/17.

Klabu ya Nice ya nchini Ufaransa nayo imeripotiwa kuwa katika harakati za kumuwania Depay, na huenda hali hiyo ikasababisha mazungumzo kati ya Man Utd na Olympic Lyon kuwa mazito.

Ndege ya Jeshi la Nigeria yashambulia kambi ya wakimbizi kimakosa
Serge Aurier: Sijazungumza Na FC Barcelona