Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uturuki zimesaini mikataba tisa ya makubaliano ya kiuchumi inayolenga katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa maendeleo baina ya nchi hizo.
Mikataba hiyo inahusisha sekta za uchukuzi, mawasiliano, habari, elimu, utalii, utafiti, viwanda, afya na ulinzi.
Akizungumza mara baada ya kusaini kwa mikataba hiyo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema ujio wa Rais wa Uturuki na ujumbe wake ni kielelezo cha ukuaji wa mahusiano baina ya Tanzania na Uturuki katika nyanja ya biashara na kimaendeleo baina nchini hizo.
Rais Magufuli amesema katika mazungumzo yake aliyofanya na Rais Recep Erdogan kuhusu ujenzi wa Reli ya Standard Gauge nchini, amemjulisha kiongozi huyo kuwa miongoni mwa wakandarasi walioomba zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kuwa ni kampuni kutoka Uturuki, hivyo endapo itashinda zabuni hiyo itasaidia kukuza uhusiano uliopo baina ya nchi hizi mbili..
Kwa upande wake Rais wa Uturuki, Recep Erdogan amesema kuwa uwepo wa mikataba hiyo baina ya Tanzania na Uturuki itasaidia kupata matokeo mazuri ya uhusiano pamoja na fursa mbalimbali za ushirikiano katika nyanja ya Kilimo, Utalii, Ulinzi, Reli ambazo zitawezesha kukuza uchumi wa mataifa hayo.
“Kiwango cha Biashara ya uwekezaji katika nchi ya Uturuki ni Dola za kimarekani 150 ambapo lengo letu ni kufika Dola za kimarekani 500” amesema Rais huyo.
Nae Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe amesema kuwa makubaliano ya mkataba baina ya Tanzania na Uturuki katika Sekta ya Utalii yatasaidia katika kutangaza vivutio vilivyopo nchini, kubadilishana wataalamu, kubadilishana taarifa na kuongeza idadi ya watalii nchini.