Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa tahadhari kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini kuwa makini na utapeli unaofanywa kupitia simu za mkononi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Meneja Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Semu amesema kuwa kuna ongezeko la matapeli wanaoghushi utaratibu wa mawasiliano na kuwalaghai watu kutuma pesa kwa simu za mkononi hivyo Mamlaka na vyombo vya usalama vinashughulikia suala hilo.
“Usitekeleze maagizo yoyote yanayohusu fedha kwa mawasiliano ya simu hata kama yanatoka kwa mtu unayemfahamu, mpigie aliyekutumia ujumbe kwa namba nyingine ili kuthibitisha’’ amesema Semu.
Aidha, ametahadharisha kuwa mtu akipokea taarifa kwa njia ya simu au ujumbe mfupi wa maandishi kuwa ametumiwa fedha kimakosa na kutakiwa kuzirudisha asifanye hivyo mpaka atakapojiridhisha na uhalali wa taarifa hiyo.
Akizungumzia matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya mitandao, Semu amebainisha kuwa kwa miezi miwili ya Novemba na Desemba 2016 jumla ya fedha iliyopita kwenye mitandao ya simu za mkononi ni shilingi trilioni 13.07 hali inayothibitisha ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya mitandao hapa nchini.