Chama cha soka nchini England (FA), kimemfungulia mashtaka meneja wa Arsenal Arsene Wenger, kufuatia kitendo cha utovu wa nidhamu alichokionyesha wakati wa mchezo wa ligi dhidi ya Burnley uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.
Wenger alionekana akimbwatukia mwamuzi namba nne wa mchezo huo Anthony Taylor, kwa kigezo cha kupinga maamuzi ya penati iliyoamuriwa ipigwe katika lango la timu yake katika dakika ya 93.
Kama hiyo haitoshi bado babu huyo alionekana akimsukuma Anthony Taylor, ikiwa ni sehemu ya kuendelea kupinga maamuzi ambayo yaliiwezesha Burnley kupata bao la kusawazisha.
FA wamempa muda Arsene Wenger kukubali ama kukataa kufanya kosa hilo, hadi itakapofika siku ya Al-khamis saa kumi na mbili jioni kwa saa za England.
Tayari wenger ameshaomba msamaha kupitia vyombo vya habari huku akisisitiza hakukusudia kufanya jambo hilo, na ilitokea kama bahati mbaya.
Kitendo cha kuomba msamaha, kinaashiria wenger amekubali kufanya kosa hilo na huenda ikawa rahisi kwa FA kumchukulia hatua za kinidhamu.
Kuna hatari ya mzee huyo akafungiwa kukaa katika benchi la Arsenal kwa zaidi ya mchezo mmoja.
Mchezo ujao Arsenal wanatarajia kupambana na Watford katika uwanja wa nyumbani na kisha wataelekea kwa majiraji zao Chelsea Februari 04.