Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani imetoa onyo kwa watu wanaoeneza taarifa za uongo za kuwepo baa la njaa nchini, kuwa ni kosa na wachukuliwe hatua mara moja.
Hayo yamesema na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni,ambapo  amesema bado kuna watu wanajichukulia mamlaka ambayo sio yao ya kueneza uongo kuwa kuna njaa nchini, hilo ni kosa kwa kuwa kwa kueneza propaganda hiyo kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini.
Ametoa  onyo hilo wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya jana Mkoani Rukwa ambako Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amemhakikishia kuwa mkoa huo hauna njaa, bali una ziada ya chakula cha kutosha.
“Nyie wenyewe mmemsikia mkuu wa mkoa (Zelothe) amethibitisha kuwa hakuna njaa mkoani hapa lakini sio hapa tu, pia mikoa ya Mbeya na Songwe wamenithibitishia kuwa hawana njaa, Sasa wapo wanasiasa uchwara wanaeneza propaganda kuna njaa, sio mamlaka yao kutangaza kuwa kuna njaa, kueneza uongo kama huo ni si sawa kwa kuwa kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini, wanastahili kuchukuliwa hatua ikiwemo kukamatwa,” amesema Masauni.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Zelothe amemwelezea Naibu Waziri Masauni kuwa hali ya kiusalama katika mkoa huo ni shwari ambapo amani na utulivu umeshamiri kwa kuwa una chakula cha kutosha.

Arsene Wenger Hatarini Kuikosa Watford, Chelsea
JPM awataka wapinzani kusoma alama za nyakati