Ndoto za kutetea ubingwa wa Afrika kwa mwaka 2017 kwa timu ya taifa ya Ivory Coast zilizimwa usiku wa kuamkia hii leo kwenye uwanja wa d’Oyem, baada ya kichapo cha bao moja kwa sifuri kilichotolewa na  Morocco.

Bao la Simba wa milima ya Atlas lilifungwa na Rachid Alioui katika dakika ya 64, na kuiwezesha Morocco kupenya kwenye hatua ya makundi na kuelekea robo fainali.

Ivory Coast ambao walikua wanapewa nafasi kubwa ya kutoa ushindani kwenye fainali za mwaka huu, kufuatia kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa michezo ya kimataifa, walishindwa kufurukuta kabisa katika harakati za kusawazisha bao hilo.

Hata hivyo huenda kocha aliewapa ubingwa wa Afrika mwaka 2015 Hervé Renard, ambaye kwa sasa ni mkuu wa benchi la ufundi la Morocco alikua chachu ya kukwamisha harakati za tembo hao wa Afrika ya Magharibi kushindwa kusawazisha, kwa kutumia mfumo uliokaba mbinu zao.

Kwa matokeo hayo Morocco wamemaliza michezo ya hatua ya makundi wakiwa na point 6 ambazo zinawaweka katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi C.

Kwa mpangilio huo Morocco anamsubiri kinara wa kundi D ambaye atajulikana mara baada ya michezo ya kundi hilo kukamilika hii leo.

Katika kundi D, michezo ya leo itakua kati ya mabingwa wa kihistoria timu ya taifa ya Misri dhidi ya Ghana na Uganda watacheza dhidi ya Mali.

Michezo yote imepangwa kuunguruma saa nne kamili usiku kwa saa za Afrika mashariki.

Shirika La Marekani Kununua Formula One
AFCON 2017: Congo DRC Mwendo Mdundo