Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali lazima ijiridhishe ni kwa namna gani itafaidika na uwekezaji katika miradi ya makaa ya mawe na chuma kabla haijaanza kwani tayari ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na muwekezaji kabla ya kuanza uzalishaji kwenye miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga.
Majaliwa amesema hayo leo Januari 26, 2017 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mundindi baada ya kukagua eneo la mradi wa chuma cha Liganga ambapo ameeleza kuwa miradi hiyo ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga inatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Ltd (SHG) ya China..
“Madini haya yana viwango vya juu vya ubora, hivyo ni lazima tuwe makini kabla ya kuanza kwa uzalishaji wake. Kwani chuma chetu ni bora na tutachimba kwa zaidi ya miaka 50,”.
“Hivyo maeneo haya ni nyeti na lazima Serikali ijipange vizuri na kujiridhisha kama vipengele vyote vya mkataba vimetengamaa ndipo mradi huo uanze,” amesema.
Majaliwa amesema mradi huo hautachukua muda mrefu utaanza hivyo wananchi wawe na subira. “Hatutaki kusikia tena suala la mikataba mibovu tunataka mikataba itakayoleta tija.
Aidha, Majaliwa amezungumzia suala la fidia kwa wananchi wanaopisha mradi ambapo amesema kabla haujaanza lazima walipwe fidia zao na tayari fedha zipo muwekezaji anasubiri ruhusa ya Serikali, amesema kuna baadhi ya watu wamejipenyeza na kutaka kuiibia Serikali kupitia suala la ulipaji wa fidia. Serikali haiko tayari kuona wananchi hao wakitumika kama madaraja ya wizi.
Amesema watu hao ambao hawahusiki na eneo hilo wamesababisha gharama za fidia kuwa kubwa, hivyo wataalam wanatathmini ili kubaini wahusika kabla ya kulipa.
“Kuna watu wanataka kuiibia Serikali kwa mgongo wenu, hili hatutakubaliana nalo. Tupo makini vumilieni inalifanyia kazi suala letu. Hakuna haki ya mtu itakayopotea,” amesema.