Watu saba, akiwamo mmoja anayedaiwa kuwa daktari bandia wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa madai ya kutengeneza kadi bandia za chanjo ya homa ya manjano na kuziuza kwa watu wanaofika hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kupata huduma hiyo.
Chanjo hizo ni zile ambazo hutolewa kwa watu ambao wanasafiri nje ya nchi kama kinga kwa ajili ya homa manjano.
Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro, amemtaja aliyejifanya daktari kuwa ni mfanyabiashara Salum Natali, mkazi wa Chanika Magengeni.
Kamanda Sirro pia amewataja watuhumiwa wengine ni walinzi watatu ambao ni Aisha Hassan, mkazi wa Vingunguti Mikoroshini, Yakobo Msenga, mkazi wa Chanika na Junith Dunstan, mkazi wa Kiwalani.
Wengine ni Oliver Bwegege mkazi wa Kigogo Mkwajuni, mjasiriamali Fredy Nyomeye, mkazi wa Chang’ombe na fundi umeme Mohamed Bwanga, mkazi wa Majohe Gongo la Mboto.
Amesema watu hao wamekamatwa Januari 16, mwaka huu baada ya mtoa taarifa kufika hospitalini hapo na kutakiwa kutoa fedha na mmoja wa watuhumiwa hao ili kupatiwa kadi hiyo ya chanjo ya homa ya manjano.
“Katika mahojiano, watuhumiwa hao walikiri kufanya kosa hilo la kughushi na kutoa kadi hizo za chanjo pasi na mtu kuchomwa sindano yenyewe ya chanjo,” amesema Sirro.
Kamishna Sirro amesema Natali alikuwa akijifanya kuwa ni daktari aliyekuwa akiwachoma watu sindano
Hata hivyo, Sirro amesema Katika tukio lingine, watu wawili wanaodaiwa kuwa majambazi wameuawa na polisi baada ya kudaiwa kuhusika kwenye tukio la mauaji Boko Basihaya, jijini Dar es Salaam.