Serikali imetoa onyo kali dhidi ya gazeti la MwanaHALISI kutokana na habari iliyochapishwa kwenye moja kati ya matoleo yake kuhusu Rais John Magufuli, isivyo sahihi.
Taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi imeeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya wahariri wa gazeti hilo kukiri kosa na kutofanya ukaidi katika hatua zote walizopitia, tofauti na ilivyokuwa awali.
Dkt. Abbasi amefafanua kuwa hali hiyo imepelekea Serikali kuwapa nafasi nyingine ingawa makosa yao yamekuwa yakijirudia.
“Mosi, wachapishaji na wahariri wa gazeti la Mwanahalisi wamepewa ONYO KALI na hatua kali zaidi zitachukuliwa endapo wataendeleza uandishi unaokiuka maadili ya kitaaluma na sheria za nchi,” imeeleza taarifa hiyo ya Serikali.
“Pili, katika habari hiyo ilichapishwa kwenye ukurasa wa mbele katika toleo lililopita, mhariri anaagizwa, bila kukosa, achapishe barua ile ile ya kuomba radhi katika ukurasa wa mbele katika toleo lijalo la Februari 6, 2017 la MwanaHALISI,” imeongeza taarifa hiyo.
Serikali imeeleza kuwa haitasita kuwachukulia hatua kali waandishi wa habari wanaoacha kuandika ukweli na kuamua kuingiza hisia zao binafsi kwenye taaluma ya uandishi wa habari.
Jana, Mhariri wa gazeti hilo aliwasilisha barua ya kumuomba radhi Rais John Magufuli akiahidi kutorudia kosa la kuchapisha habari isivyo sahihi akieleza kuwa habari hiyo ilipaswa kueleza kuhusu ofisi ya TAMISEMI badala ya Ikulu.
“Ninakiri kuwa habari hii haikuleta taswira nzuri kwa Mh. Rais na hata umma kwani ilikuwa ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na sio Ikulu. Ni kweli kabisa kwamba hakuna mazingira yoyote nanayoweza kuhalalisha kumhusisha Rais John Pombe Magufuli katika habari hii,” aliandika mhariri wa gazeti hilo.