Baada ya pambano la kihistoria lililokuwa linapikwa kati ya bingwa wa UFC asiyepigika, Conor McGregor na bingwa masumbwi wa dunia aliyestaafu bila kupigwa, Floyd Mayweather, ngoma imeguzwa kwa Manny Pacquiao.

Manny Pacquiao ambaye awali alisema kuwa Mayweather angempiga kirahisi McGregor ambaye hana uzoefu wa masumbwi bali mapigano ya ngumi, viwiko na mateke, amepokea kwa mikono miwili ombi la mpiganaji huyo na mchezo umeanza kupikwa rasmi.

McGregor alitangaza uamuzi wa kumchagua Manny Pacquiao baada ya kuona pambano kati yake na Mayweather limeishia mitini. Alisema kuwa nia yake kubwa ni kutaka kushindana na bingwa wa masumbwi ili kuchanganya ladha baada ya kukosa mpinzani kwenye ulingo wa UFC.

Akizungumzia uwezekano wa kuwepo pambano hilo, mmiliki wa ‘Top Rank’, Bob Arum amesema kuwa yeye anatamani kuliona pambano hilo na kwamba tayari Manny Pacquiao ameshakubali, kilichobaki ni makubaliano ya mgao wa fedha tu. Arum amedai kuwa pambano hilo ni rahisi sana kwa Pacquiao.

Hata hivyo, kikwazo pekee kilichopo kati ya pambano hilo ni Rais wa UFC, Dana White ambaye ameeleza kuwa MacGregor amesaini na kampuni hiyo pekee. Hivyo, ili aweze kupanda kwenye ulingo wa masumbwi ni lazima amuombe ruhusu. Aliongeza kuwa ingawa yeye anampenda Manny Pacquiao, uwepo wa Bob Arum kwenye biashara ya pambano hilo utapelekea kukataa mapema.

Akihofia kikwazo hicho, Bob Arum ameiambia TMZ kuwa yuko tayari kukaa nje ya biashara hiyo amuachie bondia huyo ajishughulikie mwenyewe, kama Rais wa UFC hapendi kumuona akihusika.

“Nakwambia, kama kikwazo pekee cha pambano kati ya Manny Pacquiao na Conor McGregor ni kwa sababu Dana (Rais wa UFC) hanipendi, nitajitoa,” alisema Arum.

Ingawa bado haijakadiliwa rasmi, pambano hili linaweza kuweka rekodi ya kuwa pambano litakaloingiza pesa nyingi zaidi kwenye historia ya masumbwi endapo litafuata mkondo wa mpango wa pambano la McGregor na Mayweather.

Serikali yatoa 'Onyo Kali' kwa gazeti la MwanaHALISI
Afrika kujiondoa mahakama ya ICC