Msanii wa muziki wa asili nchini, Mrisho Mpoto amesema kuwa yeye ni mmoja kati ya wasanii ambao wanaunga mkono harakati za Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda za kupambana na biashara ya Madawa ya kulevya.
Mpoto amesema kila mtanzania anatakiwa kumuunga mkono Makonda kwa kuwa Madawa ya kulevya tayari yameteketeza vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
“Makonda mpaka hapo alipofikia tayari amefanya kazi kubwa sana na kila mtu katika nafasi yake anatakiwa kumuunga mkono, wengi wamekuwa wakiogopa kufanya kama alivyofanya lakini yeye amefanya hivyo,” alisema Mpoto.
Mpoto amesema hayo mapema leo katika kipindi cha Tbc ambapo ameeleza kuwa huu siyo wakati wakusema kwa nini ameamua kuwaanika adharani, lakini mkumbuke mficha maradhi kifo humuumbua.
“Hata wewe kama kuna mtu unamjua unaweza kutoa taarifa katika vyombo husika ili kusaidia harakati zake ambazo ni nzuri kwa taifa letu,” – amesema Mpoto
Mpoto ameongeza kuwa ni wakati sasa watu tusiwe na tabia ya kuona madhara fulani yametokea ndipo tutangaze kusaidia, ni bora zaidi tutoe sauti zetu wakati huu ili kuwasaidia wengi zaidi. “mimi nimenza kama hivi na nitaendelea kutoa sauti ya kama ninavyofanya, Madawaya kulevya hayakubaliki,”
Aidha, Mpoto aliyewahi kuwa balozi wa amani nchini, alisema kwamba amani haipatikani kwenye utegemezi na haiendani na vitendo vya uhalifu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda hivi majuzi aliweka hadharani majina wa watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya Madawa ya kulevya hali ambayo ilipelekea askari 12 kusimaishwa kazi kutokana na tuhuma hizo huku wasanii kama Wema Sepetu, TID, Nyandu Tozzy wakiwa ndani kwa mahojiano zaidi.